Kijana wa Kiingereza ambaye alimuua kijana wa Kitanzania aliyekuwa akiishi nchini Uingereza baada ya kukasirishwa na maoni yake mabaya kwenye Facebook, amehukumiwa kwenda jela miaka 14.
Kijana huyo wa Kiingereza ambaye wakati wa tukio mwezi disemba mwaka jana alikuwa na umri wa miaka 15, alimuua kwa kumchoma na kisu kifuani kijana wa Kitanzania Salum Kombo aliyekuwa na umri wa miaka 18 ambaye alikuwa akiishi na kusoma nchini Uingereza.
Kijana huyo wa Kiingereza ambaye jina lake halikutajwa kutokana na umri wake mdogo amehukumiwa jana jijini London kutumikia kifungo jela zaidi ya miaka 14.
Kijana huyo alikuwa ni rafiki wa karibu wa Salum na chanzo cha mauaji hayo ni maoni mabaya aliyoandika Salum kwenye Facebook kuhusiana na rafiki yake huyo.
Inasemekana kwamba rafiki huyo wa Salum aliandika maoni kwenye ukurasa wake wa Facebook akionyesha hasira zake kwa kutoalikwa katika party iliyoandaliwa na rafiki zake.
Salum alijibu maoni hayo kwa kuandika maoni ya kumkashifu rafiki yake huyo ambaye kutokana na kukasirishwa kwake alitishia kumuua lakini hakuna mtu aliyetilia maanani vitisho hivyo.
Salum aliuliwa kwenye uwanja wa mpira wa kikapu karibu na nyumbani kwao. Alijaribu kujikongoja kuelekea kwao huku damu kibao zikimtiririka lakini hakufika mbali na alifariki dakika chache baadae wakati akipewa huduma ya kwanza kwenye eneo la tukio hilo.
Akijitetea mahakamani kijana huyo alisema kuwa alimshambulia Salum katika kujilinda asidhuriwe na Salum lakini hakimu aliutupilia mbali utetezi wake.
Akitoa hukumu jaji Nicholas Loraine-Smith aliamuru kijana huyo atumikie miaka 14 jela kabla ya kufikiriwa kupewa msamaha au kutolewa jela.
Salum alikuwa akisomea Sanaa kwenye chuo cha Tower Hamlets College jijini London na aliwasili Uingereza miaka saba iliyopita na alikuwa akiishi na shangazi yake jijini London.
No comments:
Post a Comment